Siku ya Veterinari Duniani 2016

Siku ya Veterinari Duniani mwaka 2016 itaadhimishwa Duniani kote tarehe 30 April 2016.

Nchini  Tanzania maadhimisho haya yanaandaliwa na Chama cha Madaktari wa Wanyama (TVA),kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi, Baraza la Veterinari, Taasisi isiyo ya kiserikali ya  Mbwa Wa Africa ,Chama cha Madaktari wa Wanyama Duninani(WVA) na Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (OIE)

KAULI MBIU: KUJIENDELEZA KITAALUMA KWA DHANA YA AFYA MOJA.
Kwa nini siku hii inaadhimishwa:
Katika karne hii ya utandawazi, magonjwa yanayoambukiza wanyama na wanadamu yanazidi kuongezeka. Inakadiriwa kuwa kati ya magonjwa mapya matano(5) yanayoibuka kila mwaka na yanayoambukiza wanadamu, matatu (3) pia yanaambukiza wanyama. Mlipuko wa ugonjwa wa Ebola uliotokea miaka ya hivi karibuni Afrika Magharibi na pia vifo vya wanadamu vinavyoendelea kutokea kutokana na Ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa vinatukumbusha uhusiano mkubwa uliopo kati ya afya ya wanadamu, wanyama na mazingira na hivyo kuwepo haja ya juhudi za pamoja kudhibiti magonjwa haya ya kuambukiza kupitia dhana ya afya moja.
Nchi zote duniani zinategemea utendaji kazi mahili wa Idara za Huduma za Mifugo kupitia sekta ya umma na binafsi, siyo tu kwa kuzuia na kudhibiti magonjwa , lakini pia kwa kuhakikisha usalama wa chakula na kuzuia madhara yanayoweza kusababishwa na vimelea mbalimbali vya magonjwa. Kwa kuzingatia ukweli huu taaluma ya Veterinari inazidi kubadilika na lazima ibadilike na hivyo haja ya wataalam hawa kujiendeleza kitaaluma kwa lengo la kuwawezesha kuwa na maarifa ya kutosha, ujuzi, uweledi na kutumia teknolojia za kisasa  kudhibiti magonjwa haya pale yanapojitokeza.
Hivyo Kauli Mbiu ya maadhimisho ya siku ya Veterinari mwaka huu imelenga kuwahimiza wataalam hawa kujiendeleza kitaaluma kwa dhana ya afya moja katika kudhibiti magonjwa yanayoambukiza wanadamu, wanyama,  kulinda usalama wa chakula na kuboresha ushirikiano na wadau wengine katika kudhibiti majanga haya.
Umuhimu wa wataalam wa taaluma ya Veterinari
Taaluma ya Veterinari inayo nafasi muhimu katika kulinda afya ya wanadamu na wanyama hapa duniani. Katika maeneo yote ya taaluma wanayo fursa na majukumu ya kuboresha afya na ustawi wa wanyama na hivyo kulinda afya ya wanadamu.
Umuhimu wa taasisi za ustawi wa wanyama katika kudhibiti magonjwa ya mifugo yanayoambukiza wanadamu na hasa Kichaa cha Mbwa
Watu wengi hufikiria taasisi za kuokoa wanyama hususan zile zinazojihusisha na uokozi wa mbwa, zimeanzishwa na watu ambao upendo wao umezidi kiwango na wangependa taasisi hizi zijihusishe na mambo muhimu kama ya elimu na kuboresha uchumi.
Je umewahi kusikia magonjwa yanayoambukiza wanyama na wanadamu? Magonjwa haya ambayo huambukiza wanyama na wanadamu yanasababishwa na virusi, bakteria, parasites na hata fangasi. Magonjwa haya yamekuwa ya kawaida. Wanasayansi wanakadilia ya kwamba  zaidi ya magonjwa  sita(6) kati ya kumi(10) yanayoambukiza wanadamu yanatoka kwa wanyama. . Mojawapo ya magonjwa hayo hatari ni Kichaa cha Mbwa . Inakadiliwa kwamba watu 1,600 hufa hapa nchini kila mwaka na hasa watoto kutokana na ugonjwa huu.
Ukizungumzia taasisi isiyo ya kiserikali ya Mbwa Wa Afrika, imeanzishwa kwa lengo la kuwasaidia mbwa wa mitaani kupata makazi mapya . Taasisi hii imewezesha mbwa 300 katika miaka mitatu(3) iliyopita kupata makazi mapya. Mbwa wengi waliofikishwa katika taasisi hii walikuwa wamejeruhiwa na walikuwa na vidonda vya kila aina  na waliwezeshwa kuendelea kuishi kutokana na matunzo yaliyotolewa na taasisi ya  Mbwa Wa Afrika. Matunzo yaliyotolewa yalihusisha  kutoa chakula, matibabu, mafunzo ya msingi ambayo yaliwafanya mbwa hawa kuwa marafiki wema kwa wamiliki wao wapya.
Taasisi hii ya Mbwa wa Afrika baada ya kutoa huduma hii kwa miaka miwili(2) , sasa hivi pia inajishughulisha na hutoaji wa chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi na taasisi isiyo ya kiserikali ya Mission Rabies ya nchini Uingereza jambo ambalo limewezesha jamii kujikinga na ugonjwa huu. Kwa sasa zaidi ya Mbwa 4,000 wamechanjwa katika kata tatu (3) za Halmashauri ya Meru , ambapo idadi hii ni sawa na  70%  ya mbwa wote waliopaswa kuchanjwa. Vilevile taasisi imeanza  kuwahasi  na kuwaondoa  vizazi mbwa kupitia upasuaji ambapo mbwa 230 wameshahasiwa au kuondelewa vizazi.
 
Ni nini tunapaswa kukumbuka wakati tunaadhimisha siku hii
Hebu fikiria utafanya nini na mbwa wachanga wanaozaliwa na mbwa wako jike. Kwa watu wengi jibu linaweza kuwa kama hutapata jirani anayependa kufuga mbwa, vichanga hivi utavitupa mitaani kwa matumaini kuwa vitajitegemea vyenyewe. Vichanga vitakavyoweza kuhimili misukosuko na hatimaye kuweza kujitegemea ndiyo baadae utakutana nao mitaani wakiwa mbwa wakubwa na ambao watakutisha wakati wakizunguka kutafuta chakula, kulinda vichanga vyao na wakigombania majike.
Ili kuweza kudhibiti idadi ya mbwa katika eneo husika, kuondoa kizazi kwa mbwa jike au kuhasi mbwa dume kunaweza kusaidia. Programmu ya kuhasi au kuondoa kizazi haizui kudhibiti magonjwa, lakini inasaidia kupunguza idadi ya mbwa na hivyo kupunguza tatizo la mbwa wa mitaani na gharama za chanjo. Vilevile program hii inasaidia ustawi  wa wanyama hawa na huwafanya kuishi wakiwa na afya njema na pia maisha marefu kwa vile hawajihusishi kuzurura wakitafuta majike mitaani na watabaki nyumbani wakikulinda wewe na familia yako. Aidha unapaswa kutambua kwamba mbwa ni marafiki wema na wakipendwa na wao watakupenda na kukulinda..
Wengi wetu bado tunaamini kwamba tunapomfunga mbwa mnyororo au kumfungia mahali siku nzima atakuwa mkali sana na hivyo ataweza kufukuza wezi na vibaka wakati wa usiku. Lakini hebu jiulize je utamsaidia rafiki ambaye anakufanyia matendo ya kukufunga kwenye mnyororo au kukufungia ndani ya chumba siku nzima? au utamsadia rafiki yule ambaye kila wakati unakuwa naye, ambaye anakupa maji na chakula kila mara. Hebu kumbuka mbwa uliyekuwa naye wakati ulipokuwa mtoto, ambaye alikuwa akikufuata shuleni ulipokuwa ukiondoka nyumbani, je haingekuwa vyema kama ungekuwa bado unaye?
Ndiyo unaweza kusema watu wanaojihusisha na ustawi wa wanyama wamezidisha upendo wao kwa wanyama, lakini ikumbukwe watu hawa wanasaidia kuifanya jamii kujikinga na magonjwa kama ya kichaa cha mbwa na hivyo tunapaswa kuthamini mchango wao.
 
TUNAWATAKIA MAADHIMISHO MEMA YA SIKU YA VETERINARI 2016

 

Share on FacebookTweet about this on TwitterShare on LinkedInShare on Google+Email this to someone